Zitto Kabwe: Hali ya Uchumi ni Mbaya, Watanzania Wamepoteza Matumaini.


Sehemu ya 1 ya Hotuba ya ndugu Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (MB) kuhusu Mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kwa mwaka 2017/18]

"Mheshimiwa Spika,

Tangu mwezi Novemba mwaka 2015 nchi yetu ilipata Serikali mpya iliyoanza kazi kwa kasi kubwa haswa katika maeneo ya kupambana na rushwa, ufisadi na kuongeza mapato ya Serikali. Wananchi walikuwa na matumaini makubwa sana kutokana na mwanzo huu, na hata ufanisi katika utendaji wa kazi Serikalini ulianza kuboreka.

Bahati mbaya, leo tunapokutana kujadili utendaji wa Serikali wa mwaka uliopita na kupanga Bajeti ya mwaka unaofuata wa fedha matumaini hayapo tena, kuna hali kubwa ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi.

Maeneo mengi ya nchi kuna uhaba mkubwa wa chakula na badala ya Serikali na hasa Rais kuwa matumaini Kwa wananchi akiwa Comforter In Chief, kumekuwa na maneno makali ya kuwakatisha tamaa wananchi. Bei za vyakula nchini zimepanda mno kiasi cha wananchi kushindwa kumudu chakula ili waweze kufanya kazi na kukuza Uchumi.

Taarifa za Serikali kupitia ripoti za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake juu ya hali ya Uchumi ya nchi yetu (Quartely Economic Review na Monthly Economic Review) kwa mwezi wa Disemba 2016 zinaonesha kuwa kuna mfumuko mkubwa mno wa bei za Vyakula, hasa Chakula Kikuu kwa Watanzania - Mahindi, ambapo bei ya chakula hicho kikuu nchini imepanda kwa zaidi ya 30% na kupandisha mno gharama za maisha za wananchi wote nchi nzima.

Leo bei ya kilo moja ya mahindi nchini iko sawa au ni zaidi ya bei ya kilo moja ya mchele kwenye miji mbalimbali nchini, sukari bei juu, mafuta ya kula bei juu nk. Kwa wakazi wa mjini hata bei ya gesi kwaajili ya kupikia majumbani imepanda, wananchi wamerudia matumizi ya mkaa, tujiandae na uharibifu wa misitu nchini.

Jana Ofisi ya takwimu ya Taifa imetoa Taarifa ya kuonyesha kuwa Mfumuko wa Bei umepanda kwa kasi na sasa umefika asilimia 6.4 Kwa mwaka unaoishia Machi, 2017. Ibara ya 20 ya Hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa bungeni inaonyesha mfumuko wa bei wa asilimia 5.2 kwani wametumia takwimu za mwezi Desemba, 2016.

Ukuaji wa sekta binafsi umedorora na kushuhudia biashara maelfu kwa maelfu zikifungwa na kusababisha ajira nyingi kupotea na ajira chache kutengenezwa. Katka Ibara ya 26 ya Hotuba ya Waziri Mkuu inaonekana kuwa ajira 418,000 zilizalishwa mwaka 2016/17. Lakini Waziri Mkuu hakulieleza Taifa kuwa Hivi sasa Watanzania 1.6m wanaingia kwenye soko la Ajira kila mwaka. Pia Waziri Mkuu hakueleza Taifa ni ajira ngapi zimepotea Kwa viwanda kufungwa au kupunguza uzalishaji na biashara kufungwa. Manispaa ya Ilala peke yake imefunga biashara 2900 na hivyo kupoteza chanzo cha mapato ya Manispaa. Lakini hata mikopo ya Kibenki kwa sekta binafsi imepungua mno, ikiwa ni kiashiria cha mdororo wa sekta binafsi.

Matamko ya viongozi wakuu wa Serikali kuhusu mwelekeo wa Uchumi yanatuma ujumbe hasi kuhusu uwekezaji wa mitaji nchini, na hivi sasa kila mwekezaji kwenye macho ya Serikali anaonekana mpiga dili. Juhudi zote za kuhamasisha uwekaji wa mitaji nchini zilizofanywa tangu Serikali ya awamu ya tatu, zimefutwa katika mwaka Mmoja tu wa Serikali ya awamu ya tano. Hali ni ya kusikitisha sana.

Tatizo jengine kubwa ni suala la ajira, ukiondoa ajira zilizopotea kwa mdororo wa sekta binafsi, lakini pia hakuna ajira mpya serikalini tangu awamu ya tano iingie madarakani. Vijana mbalimbali waliomaliza masomo yao ya Ualimu, Utabibu, Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvivu bado wako mtaani bila ajira kwa mwaka sasa. Hata walioajiriwa mwanzoni ajira zilisitishwa kwa kisingizio cha uhakiki wa watumishi wa Umma.

Yote hayo yana athari kwenye uchumi wa nchi, yamepunguza kipato cha wananchi, yamechangia ugumu wa maisha. Yamefuta matumaini waliyokuwa nayo watanzania na yamewakatisha tamaa. Bunge letu lina wajibu wa kuhakikisha Serikali inarelebisha hayo".

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Bungeni Dodoma
April 11, 2017

No comments

TUFATILIE TWITTER

Powered by Blogger.